Imetimia miaka 100 tangu kutokea kwa mama Bikira Maria huko fatma, tunakumbuka miaka 100 tangu kulipotokea tukio muhimu la mama Bikira Maria kuwatokea watoto watatu wa Fatima LUSIA, FRANSISCO na YASINTA.

Na. Juvenalis Ngowi & www.nimeonjapendo.com


Kesho tarehe 13 Mei 2017 ni siku ambapo kanisa kote ulimwenguni linaadhimisha miaka 100 tangu Mama yetu Bikira Maria alipowatokea kwa mara ya kwanza watoto watatu Fatima, na ni siku ambapo Baba Mtakatifu Francis anatarajiwa kumtanganza mtoto wa mwisho kufariki (Sr. Lusia) kuwa mtakatifu baada ya wadogo zake wawili kutangazwa miaka 17 iliyopita.


Kwa umuhimu wa tukio hili, www.nimeonjapendo.com kwa ushirikiano na msaada wa Juvenalis Ngowi inakuletea simulizi refu na la kusisimua sana la namna watoto wale walivyotokewa na Bikira Maria, pamoja na miujiza ya ajabu iliyoambatana na matokeo yale.

Tarehe 13 Mei 1917 Bikira Maria aliwatokea watoto watatu wa parokia ya Fatima iliyoko Ureno. Watoto hao ni Lusia, Fransis na Yasinta. Fransis na Yasinta walikuwa watoto wa baba na mama mmoja. Lucia alikuwa binamu yao na ndiye aliyekuwa mkubwa zaidi kiumri.

Kwanza tumtazame Lusia kwa kifupi kabisa.

Alizaliwa 30/03/1907 huko Ureno. Alikuwa mtoto wa mwisho katika familia yao ya watoto saba. Katika utoto wake kazi kubwa ya nyumbani aliyofanya ilikuwa kuchunga mifugo ya familia. Alianza kujifunza kusoma na kuandika baada ya matokeo ya Bikira Maria ambaye alimtaka ajifunze kusoma. 

Lusia ana umuhimu wa pekee katika matokeo ya Fatima kwa kuwa yeye ndiye hasa aliyekuwa akipewa ujumbe na Bikira Maria wakati wa matokeo na kwa namna ya pekee ndiye aliyekabidhiwa zile siri tatu. Baada ya matokeo Lusia alijiunga na utawa wa masista wa Mt. Dorotea ingawa baadae kwa ruhusa ya Askofu alibadili shirika na kujiunga na shirika la wakarmeli kwa kuwa alitamani upweke na shirika la wakarmeli lilitoa nafasi hiyo ya upweke. Tangu utoto Lusia alilelewa vyema kiimani na aliweza kupata komunio ya kwanza akiwa na miaka sita tu. Alipopokea komunyo takatifu alipiga magoti na kusali "...Ee Bwana, unifanye mtakatifu, uulinde moyo wangu uwe safi daima kwa ajili yako tu".

Sasa tumwangalie Yasinta kwa ufupi.

Yasinta alikuwa binamu wa Lusia. Alilelewa katika misingi bora ya kikatoliki. Yeye na kaka yake FranSis walimpenda sana binamu yao LuSia kiasi kwamba walimbembeleza mama yao awaruhusu kuchunga mifugo wakiwa bado wadogo ili waweze kufuatana naye. Yasinta alikuwa mwepesi kukasirika na ikitokea amechokozwa kidogo angejikunyata pembeni na kununa. Lakini kwa ujumla alikuwa na tabia njema. Mama yake alimlinda kwa kuangalia kwa uangalifu anacheza michezo gani na anachezea wapi na anacheza na akina nani.

Lusia kwa vile ndiye alikuwa mkubwa, alizoea kuwasimulia binamu zake hawa habari za Biblia na katekisimu. Katika michezo yao (Lusia, Fransis na Yasinta), walishindana kuhesabu nyota. Waliziita nyota taa za Malaika na mwezi taa ya Bikira Maria.

Yasinta akiwa na umri mdogo sana aliruhusiwa kurusha maua kwa Yesu wakati wa sikukuu ya Ekaristi. Ajabu ni kuwa wakati wenzake wanarusha maua, Yasinta hakuweza kurusha. Alibaki kumwangalia tu padre. Alipoulizwa baadae kwa nini hakurusha maua alisema hakumwona Yesu aliyeambiwa amrushie maua! Ilibidi Lusia amfundishe kuwa Yesu amejificha kwenye Ekaristi takatifu.

Kama nilivyoeleza, Yasinta na Fransis walianza kuchunga mifugo wakiwa na umri mdogo sana. Wakiwa machungani walicheza michezo mingi lakini wakubwa nyumbani waliwaagiza kuwa kila mchana wasali rozari. Walisali rozari kitoto na mara nyingi walisema tu "salamu Maria" bila kumalizia sala yote ili wawahi kucheza.

Tabia za Fransis

Mara ya kwanza kusoma kuhusu Fransis zaidi ya miaka 20 iliyopita, nilipata picha kuwa Fransis alikuwa mtoto mtukutu! Sababu hasa ya kujijengea picha hii ni ukweli kuwa Mama alipowatokea walimuuliza ikiwa watakwenda mbinguni. Mama akawaambia Yasinta atakwenda mbinguni katika kitambo kifupi. Lusia atabakia duniani kwa muda mrefu zaidi. Wakamuuliza kuhusu Francis. Mama alikaa kimya kidogo halafu akasema Fransis atakwenda mbinguni lakini itamlazimu kusali sana.

Hata hivyo nilipokuja kusoma maelezo ya Lusia kuhusu tabia ya Fransis nilijua kuwa Fransis alikuwa mtoto mpole. Lusia anasema usingeweza kujua kuwa Fransis na Yasinta walikuwa ndugu wa tumbo moja kutokana na utofauti wa tabia. Yasinta alikuwa motomoto na asingekubali kuonewa. Fransis alikuwa hapendi fujo na alikuwa tayari kupoteza haki zake kuliko kushirki kwenye mzozo. Mara nyingi alishiriki michezo ili tu kumridhisha dada yake Yasinta.

Wakati wa kutokewa kimsingi yeye Fransis aliona yaliyotokea lakini hakusikia sauti. Na baada ya kutokewa alifanya bidii kubwa kutoa sadaka za kujinyima. Watoto hao kwa mfano wakikaribishwa kinywaji angetoroka ili asinywe na hivyo kutolea jambo hilo kama sadaka ndogo. Pia alikuwa akuwatoroka wenzake na kwenda kujificha ili aweze kusali. Alitamani sana kwenda mbinguni ili akaone uzuri walioonyeshwa walipotokewa.

Malaika anawatokea kuwaandaa kabla ya hawajatokewa na Bikira Maria

Bila kujijua, watoto hawa waliandaliwa vya kutosha kabla ya kumuona Mama wa Mungu. Pengine ni watu wachache tu wanaofahamu kuwa kabla ya watoto hawa kutokewa na Bikira Maria walitokewa na malaika mara tatu kwa nyakati tofauti.

Hebu tuangalie tokeo la kwanza la Malaika.

Kwa kuwa watoto hawa hawakuwa wamekwenda shule, Lusia anasema hawezi kufahamu ilikuwa tarehe ngapi walipotokewa na Malaika kwa mara ya kwanza ila anafahamu ilikuwa mwaka 1916 msimu wa kipupwe. Nchini Ureno kipupwe huwa ama mwezi Novemba mpaka Desemba, au Januari mpaka Machi. Kwa hiyo inawezekana ilikuwa mwanzoni mwa mwaka 1916 au mwishoni mwa mwaka huo.

Watoto walikuwa wamemaliza kupata mlo wao wa mchana na wakasali kama ilivyokuwa desturi yao. Wakiwa porini waliona kitu chenye umbo la mvulana chenye uangavu sana. Kitu kile kilizidi kuwakaribia na kikaonekana vizuri zaidi kama mvulana aliye katika utukufu mkubwa.

Watoto walipatwa na mshangao na kuduwaa. Kiumbe yule alipowafikia akasema: "Msiwe na hofu mimi ni Malaika wa Amani. Tafadhali salini pamoja nami." Malaika yule akapiga magoti akainama hadi paji la uso likagusa chini. Watoto wale kwa nguvu wasiyoijua nao wakafanya kama yule Malaika.

Malaika akasali na watoto wakarudia maneno yale. Sala yenyewe ilikuwa hii; "Ee Mungu wangu nakusadiki, nakuabudu, nakutumainia, nakupenda. Ninakuomba msamaha kwa ajili ya wote wasiokusadiki, wasiokuabudu, wasiokutumainia na wasiokupenda."

Akarudia sala hii mara tatu kisha akawaagiza waisali sala hiyo mara kwa mara na kuwahakikishia kuwa Yesu na Maria wanapenda kusikiliza maombi yao.

Baada ya Malaika kuondoka watoto wale wakawa kama hawajitambui lakini walihisi hali ya uwepo wa Mungu kati yao. Wakairudia ile sala tena na tena. Walizama katika hali ya kiroho kiasi kwamba ilikuwa vigumu hata kuzungumza wao kwa wao hadi kesho yake. Wala hawakumsimulia yeyote kilichowatokea.

Malaika anawatokea mara ya pili

Hatuna kumbukumbu ya tarehe jambo hili lilipotukia lakini ni kabla ya Mama kuwatokea. Ilikuwa mchana wa joto kali na watoto walikuwa wameamua kurudisha kondoo nyumbani. Baada ya kurudisha mifugo watoto waliamua kutafuta kivuli wapumzike. 

Loh! Mara wakajiona wakiwa na yule Malaika aliyewatokea kitambo kilichokuwa kimepita.

Malaika akawauliza, " mnafanya nini hapa?". Akazidi kuwaambia wasali sana na kutolea sadaka kwa kuwa Yesu na Maria walikuwa na matarajio makubwa kutoka kwa watoto wale.

Watoto wakauliza watoe sadaka gani? Malaika akawajibu kuwa watolee chochote wanachoona kwa mawazo yao kinafaa kwa sadaka. Watolee sadaka kwa malipizi ya dhambi na kwa ajili ya uongofu wa wakosefu. Pia Malaika aliwataka watoto wale wawe radhi kupokea mateso ambayo Yesu angependa wayaonje.
Maneno hayo yalinasa katika akili na utashi wa watoto wale kiasi kwamba kuanzia siku hiyo walikuwa wakitolea kila jambo linaloweza kuwaumiza katika maisha ya kawaida kama sadaka yao. 

Malaika anawatokea kwa mara ya tatu

Kitambo kirefu kiasi kilikuwa kimepita tangu tokeo la pili la Malaika. Watoto walikwenda kuchunga kondoo kama kawaida. Wakaamua kutafuta sehemu ya kusali. Wakapata pango zuri eneo lenye miti ya mizeituni. Wakapiga magoti na kuinama hadi uso ukagusa ardhi kisha wakasali ile sala yao ya Mungu wangu ninakusadiki, ninakuabudu.....

Mara wakaona mwanga wa ajabu juu yao. Wakashtuka kuona kulikoni? Wakamwona yule Malaika "wao" akiwa ameshika kalisi na hostia ikiwa juu ya kalisi. Hostia ilikuwa inavuja matone ya damu yakidondokea ndani ya kalisi.

Malaika akaachia kalisi na hostia vikabaki angani yeye akawasogelea watoto na kupiga nao magoti akawafundisha sala hii:

"Ewe Utatu Mtakatifu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ninakutolea Mwili na Damu takatifu, Roho wa umungu wa Yesu Kristu anayekuwemo kweli kabisa katika Tabernakulo zote duniani, kama malipizi ya matusi, ya makufuru na ubaridi vinavyomchukiza yeye mwenyewe. Na kwa ajili ya mastahili yasiyo na mipaka ya Moyo wake Mtakatifu na ya Moyo Safi wa Maria".

Halafu Malaika akaitwaa ile kalisi na Hostia mikononi mwake na akawagawia wale watoto akisema:

"Kula na kunyweni Mwili na Damu ya Yesu Kristu anayetukanishwa vikali na watu wasio na shukrani. Fanyeni malipizi kwa dhambi zao na mumtulize Mungu wenu".

Watoto wale walibaki mahali pale kwa kitambo kirefu hadi pakaanza kuwa giza. Wakaenda nyumbani.


Sasa watoto wanatokewa na Bikira Maria huko shimo la Iria

Tarehe 13/05/1917 watoto walianza siku yao kama kawaida. Walipanga siku hiyo wataenda kuwalisha kondoo sehemu inayoitwa Shimo la Iria (Kova da Iria). Eneo hili lilikuwa umbali mrefu kutoka nyumbani na njia ilikuwa mbaya. Hivyo walifika malishoni mchana wa saa sita hivi.

Wakati wakiendelea na kuchunga kondoo walikuwa pia wakicheza michezo yao ya kitoto.

Ghafla wakaona mwanga mkali. Wakadhani ni radi na pengine mvua ingenyesha. Lusia akawashauri binamu zake warudi nyumbani mvua isije wakuta huko machungani.

Walianza kuwaswaga kondoo haraka wakishuka kilima. Mwanga mkubwa ukaonekana tena. Wakadhani radi inaendelea. Walipozidi kwenda mbele wakamwona Bibi mzuuuuuuri anaelea juu ya mti mchanga. Alikuwa amevaa mavazi meupe na alikuwa mwangavi kuliko jua!

Watoto walisimama mbele ya huyo Bibi kama hatua mbili-tatu hivi. Wakawa ndani kabisa ya mwanga uliotoka kwa yule Bibi. Yule Bibi akawaambia "Msiogope sitawadhuru". Wakamuuliza " umetoka wapi?" Akawajibu, "Nimetoka mbinguni".

Lusia akauliza, "Unataka nini kwangu?" Yule Bibi akawaambia anataka watoto wale wafike sehemu ile tarehe ya 13 ya kila mwezi. Na kwamba baadae atawaambia yeye ni nani na anataka nini, Kisha atawarudia kwa mara saba.

Yule Bibi aliposema ametoka mbinguni na baada ya maelezo aliyowapa, Lusia akauliza "je nitakwenda mbinguni?". Akajibiwa kuwa atakwenda. Akauliza na Yasinta je? Jibu likawa ndio atakwenda. Akauliza tena na Fransis atakwenda? Bibi akamjibu atakwenda lakini shuruti asali rozari nyingi sana.

Lusia akakumbuka rafiki zake wawili waliokuwa wamefariki siku si nyingi. Akamuuliza yule Bibi, Maria de Naves yupo mbinguni? Akajibiwa yupo mbinguni. Huyu alifariki akiwa na miaka 16 hivi. Lucia akazidi kudadisi kuhusu rafiki yake mwingine aitwae Amelia ikiwa naye yupo mbinguni. Yule Bibi akasema huyo yuko toharani na atakaa huko hadi mwisho wa dunia. Huyu alifariki akiwa na umri kati ya miaka 18 na 20 hivi.

Bibi yule mzuri akauliza ikiwa watoto wale wako tayari kujitolea nafsi zao na kuvumilia mateso yote Mungu atakayopenda kuwatumia kama tendo la malipizi kwa dhambi zinazomchukiza na wongofu wa wakosefu. Watoto wakakubali. Bibi akawaambia kuwa watapata mateso mengi lakini neema ya Mungu itakuwa faraja yao.

Alipotamka maneno "NEEMA YA MUNGU NDIYO FARAJA YENU" akafumbua viganja vyake akawashirikisha mwanga wa nguvu kamili uliotoka viganjani na kupenya hadi kwenye nyoyo zao. Kwa nguvu ya mwanga huo wale watoto walijiona ndani ya Mungu na kwa kujiona ndani ya Mungu waliweza kujiona wenyewe vizuri zaidi kuliko mtu unavyojiona kwenye kioo.

Kwa nguvu ya ajabu walijikuta wakipiga magoti na kusali ile sala ya "Ewe Utatu Mtakatifu ninakuabudu. Ee Mungu wangu, Mungu wangu ninakupenda katika Sakramenti Kuu."

Baada ya dakika chache Bibi akawaambia, "Salini Rozari kila siku kwa ajili ya kupata amani duniani na vita imalizike". Akiisha kusema hayo akapaa kwenda zake akatoweka angani.

Bikira Maria anawatokea watoto kwa mara ya pili

Kama nilivyosimulia hapo awali, yule Bibi aliwaelekeza watoto wafike pale shimo la Iria kila tarehe 13. Hivyo tarehe 13 Juni 1917 watoto walitii amri na kwenda eneo la tukio.

Ingawa walikuwa wamekubaliana wafanye siri kuhusu yaliyowatokea, Yasinta alishindwa kuvumilia na akatoa siri bila kutaka. Alivutwa mno na uzuri wa yule Bibi hivi akawa anashindwa kujizuia kuzungumza na siri ikafichuka!

Kwa kuwa baadhi ya watu walishafahamu jambo hili ingawa wengine waliwaona watoto wale kuwa wazushi, siku hiyo ya 13 Juni 1917 kulikuwepo pia watu wengine kadhaa nao wakitaka kushuhudia kitakachotokea.

Wakiisha kufika eneo la tukio walianza kusali rozari. Walipomaliza tu kusali rozari mvua na radi vilianza. 

Muda mfupi baadae yule Bibi aliwatokea juu ya mti ule ule aliowatokea mara ya kwanza. Lusia akamuuluza tena, " Unataka nifanye nini?". Bibi akawajibu kuwa anataka wafike pale tena tarehe 13 ya mwezi utakaofuata.

Aliwataka pia wajifunze kusoma na kwamba atawaambia baadae anachokitaka kwa watoto hao. Lucia alimwomba amponyeshe mgonjwa mmoja aliyekuwa akiumwa. Bibi akasema mgonjwa yule angepona mwaka ule kama atatubu dhambi zake. Lusia akazidi kuongea na Bibi na kumuomba awapeleke mbinguni. Bibi akasema Yasinta na Fransis watakwenda siku si nyingi bali Lucia atabaki duniani kwa muda mrefu zaidi kwa kuwa angepaswa kufanya kazi ya kumtambulisha Bibi kwa watu ili wampende na angeanzisha ibada kwa Moyo Safi wa Bibi.

Kisha Bibi aliwafumbulia viganja vyake kama ilivyokuwa katika tokeo la kwanza na mwanga ule wa ajabu ukawajia nao wakazama ndani ya Mungu. Yasinta na Fransis walimulikwa na sehemu ya mwanga ulioelekea mbinguni lakini Lusia alimulikwa na mwanga ulioelekea ardhini.

Katika kiganja cha mkono wa kulia ulionekana moyo uliozingirwa na miiba na kuuchoma. Watoto wakatambua ulikuwa Moyo Safi wa Bibi. Na kwamba ulikuwa unatukanwa na sasa ulihitaji malipizi.

Bibi awatokea watoto kwa mara ya tatu, umati mkubwa zaidi wahudhuria, watoto waoneshwa siri ya kwanza

Habari za matokeo ya Bibi yule mzuri kwa watoto zilizidi kuenea. Wapo waliosadiki na wapo waliozipinga wakiwaona watoto wale kuwa ni wazushi tu.

Habari kwamba watoto wale walielekezwa waende tena kule shimo la Iria tarehe 13 Julai zilisambaa sana. Siku hiyo eneo la tukio lilikuwa na watu wengi sana. Watoto walipofika hapo watu walishafurika wakisali rozari. 

Muda mfupi baada ya watoto kufika ukatokea tena ule mwanga mithili ya radi. Watoto wakamwona yule Bibi juu ya mti ule ule.

Lusia akamuuliza tena Bibi anataka nini? Bibi akawajibu; "Nataka mfike hapa tarehe 13 ya mwezi kesho. Endeleeni kusali Rozari kila siku kwa heshima ya Bibi yenu wa Rozari; kwa kusudi la kupata amani duniani, na vita imalizike, kwa sababu hakuna mwingine awezaye kuwasaidia ila yeye tu."
Lusia akamwomba yule Bibi ajitambulishe na pia akamuomba afanye muujiza kusudi watu wakubali wametokewa kweli. Bibi akawaambia waendelee kufika eneo lile kila tarehe 13 na katika mwezi Oktoba angewaambia yeye ni nani na katika mwezi huo huo atafanya ishara itakayoonekana kwa watu wote ili wasadiki.

Bibi akasema tena maneno haya; "Jitoleeni nafsi zenu sadaka kwa ajili ya wakosefu, na semeni mara nyingi sala ifuatayo wakati ule mnapotolea sadaka; “ Ee Yesu, ni kwa ajili ya kukuonyesha mapendo; ni kwa ajili ya wongofu wa wakosefu; na kwa ajili ya malipizi ya dhambi zinazotendwa dhidi ya Moyo Safi wa Maria".

Baada ya Bibi yule kuwaambia watoto wajitolee nafsi zao kwa ajili ya wakosefu na kuwafundisha ile sala, alifumbua mikono yake kama alivyofanya miezi miwili iliyotangulia. Tofauti ni kuwa wakati huu mionzi ilipenya ndani ya ardhi.

Watoto wakaona kwa macho yao jambo ambalo ndilo likawa siri ya kwanza kati ya siri tatu za Fatima. Siri hii iliwatisha sana sana sana, hofu yao ikawa dhahiri na umati wote ukaishuhudia waziwazi.

Watoto walitetemeka kwa hofu kuu na Lusia anasema baadaye watu walimweleza kuwa alilia kwa sauti ya kutisha na hofu. 

Mambo yaliwatisha mno watoto hivyo wakamtazama Bibi kama vile kuomba msaada. Bibi akawatazama kwa wema uliochanganyika na uchungu. Kisha akasema nao kidogo juu ya siri ile.

Kukawa kimya kwa kitambo kifupi kisha Lusia akauliza endapo Bibi alitaka kitu kutoka kwake. Bibi akasema; "Hapana, kwa leo sihitaji kitu chochote kingine kwako".

Bibi akapaa juu hadi akatoweka upeo wa macho yao.

Familia, Serikali, raia, na vyombo vya habari wapinga vikali habari za kutokea kwa Bikira Maria

Habari za kutokea kwa Bibi zilisambaa sana na kufika hadi maeneo ya mbali. Pia ilielezwa kuwa Bibi alikuwa amewapa watoto siri tatu maalum. 

Siyo watu wote walioamini habari hizi za watoto kutokewa na Bibi yule mzuri. Hata familia ya Lusia haikumwamini hata kidogo. Mama yake alimuita muongo na akamtaka akanushe taarifa hizo.

Lusia alibaki imara licha ya ukweli kuwa kuna wakati alipata kishawishi kuwa labda anayewatokea ni shetani.

Upande wa serikali nako kulikuwepo mzozo. Mkuu wa wilaya alitaka watoto wampe siri walizoambiwa na Bibi, na akawakataza watoto wasirudi tena kule eneo la tukio. Watoto walikuwa jasiri na hawakutetereka. Walishikilia msimamo wao.

Kadiri tarehe ya tukio ilivyokaribia ndivyo mkuu wa wilaya alivyozidisha vitisho kwa watoto.

Wakati mmoja alitoa amri kwamba watoto waende ofisini kwake kuhojiwa. Wazazi wa Fransis na Yasinta walikataa watoto wasiende kwa kuwa ni wadogo na ilikuwa safari ya umbali mrefu, na hakukuwepo usafiri wa gari wala treni, badala yake baba yao akasema angeenda kwa niaba yao. Lakini wazazi wa Lusia walisema binti yao aende mwenyewe na ikijulikana amesema uongo aadhibiwe.

Lusia alianza safari hiyo ndefu kwa kutumia punda ikiwa ndio mara yake ya kwanza. Njiani alianguka mara kadhaa. Huku nyuma Fransis na Yasinta walikuwa na huzuni kali kwani walihofu labda Lucia atakwenda kuuwawa.

Lucia alipofika alihojiwa. Kwanza mkuu wa wilaya alikuwa mpole akimuahidi zawadi ili atoe siri na pia asiende tena eneo la tukio. Lusia alibaki imara. Hapo ndipo vitisho vilifuata. Hata katika vitisho hivyo hakubabaika. Mkuu wa wilaya alikasirika akamfukuza arudi nyumbani.

Siku ya miadi kati ya watoto na Bibi zilikaribia sana. Watu kutoka pande mbalimbali walianza kuwasili Fatima wengi wakitaka wawepo eneo hilo Bibi atakapotokea. Wengine walikuwa wakiwatafuta watoto wawape maombi yao kumpelekea Bibi.

Eneo la tukio lilikuwa ni shamba la familia ya Lucia ambapo walilima mazao ya chakula kama vile njegere.

Wingi wa watu uliharibu sana mazao shambani. Nyumbani kwa Lusia wakawa wanamkejeli kwa kumuambia huyo Bibi akija amletee na chakula. Lusia akavumilia yote.
Serikali nayo haikukata tamaa katika kujaribu kuwarubuni watoto wale watoe siri. Pia magazeti yasiyopenda kanisa yalisambaza propaganda kuwa kile kilichosemwa kuwa ni kutokewa kwa Bibi ni uongo. Wengine wakasema ni ujanja wa padre kupata fedha. Alimradi walijitahidi kupotosha kilichokuwa kimetokea.

Serikali yawateka watoto ili kuzuia tokeo la nne

Tarehe 13 August ikafika. Ndio siku Bibi aliwaambia watoto waende kule Shimo la Iria. Watu wengi walishafika. Mkuu wa wilaya naye akafika nyumbani kwa watokewa akitaka naye kuwaona! Alikuwa na gari la kukokotwa. Eti naye alitaka kuona muujiza.

Baada ya kuonana na kumsalimia paroko, aliomba watoto waingie kwenye gari yake. Gari ikachukua uelekeo kama inaenda eneo la tukio lakini ghafla ikabadili uelekeo na yule mkuu wa wilaya akawahadaa watoto kuwa wanakwenda kumuona kwanza padre mwingine wa eneo jingine. Ili wageni waliofika Fatima wasiwaone watoto, aliwafunika kwa matambara. Watoto walikuwa wametekwa!

Mkuu huyu wa Wilaya akawachukua hadi nyumbani kwake. Wakohojiwa huku wakishawishiwa kwa kila namna watoe siri walizoambiwa na Bibi. Watoto walikataa katakata kueleza siri walizoonyeshwa na kuambiwa.

Watoto wanatupwa gerezani na kuteswa ili watoe siri

Mkuu wa wilaya alipoona ameshindwa kupata alichotaka kutoka kwa watoto wale, aliamuru watupwe gerezani. Watoto wale walikubali kwenda gerezani kuliko kutoa siri walizoambiwa na Bibi.

Wakiwa gerezani vitisho viliendelea. Kuna wakati watoto walitenganishwa na wakati mwingine waliwekwa pamoja.

Muda ulizidi kusogea na hakukuwepo dalili kuwa wataachiwa hivyo walikuwa na huzuni kwa kuwa wasingeweza kwenda pale Bibi alipoweka miadi ya kukutana nao.

Watoto wakaonywa kama hawasemi siri watakaangwa kwenye mafuta yanayochemka wakiwa hai. Watoto hawa wakawa tayari kuuwawa kuliko kutoa siri. Yasinta alikuwa akilia sana. Lusia akamuuliza kwa nini analia? Akajibu kuwa anasikitika atakufa bila kumuona mama yake. Fransis alimtuliza sana. Lusia akamkumbusha kuwa yampasa kutolea uchungu ule na mateso kwa ajili ya wongofu wa wakosefu. Kuna wakati Fransis alisema afadhali wauwawe ili waende mbinguni mapema.

Wafungwa wengine mle gerezani waliwashangaa wale watoto. Wakawaambia kwa nini wapate taabu vile? Wakawaambia semeni hizo siri na shida zenu zitakwisha. Watoto wakabaki bila kubadili msimamo.

Watoto wakaitwa mmoja mmoja tena ili kutishwa. Yasinta alipoitwa, Fransis akamwambia Lusia; "Mimi nitasali sala ya salamu Maria ili Yasinta asiogope". Wote wakahojiwa na kutishwa sana. Ikawa hakika kabisa sasa hawataweza tena kwenda shimo la Iria siku hiyo wakamuone Bibi.

Watoto wakakata shauri wasali rozari kule kule gerezani. Yasinta akavua medali yake akamuomba mfungwa mmoja aitundike kwenye msumari ukutani pale gerezani. Watoto wakapiga magoti na kuanza kusali. Wafungwa wengine wakajiunga nao kwa sala.

Walipomaliza kusali wafungwa wengine waliwahurumia watoto wale wakataka kuwapotezea mawazo hivyo wakaanza kupiga muziki na kucheza dansi. Yasinta alikuwa mpenzi wa muziki hivyo ilionekana kumsaidia kidogo.

Watoto wakosa kwenda Shimo la Iria mwezi Agosti, lakini Bibi awatokea katika eneo jingine

Muda ulikuwa umesogea sana watoto wakiwa bado kule gerezani na hakukuwepo dalili yoyote ya kuwachia watoto waondoke ili waende kule shimo la Iria. Wakawa wanasononeka sana kuwa hawatamwona yule Bibi.

Fransis akiwa katika majonzi akasema: "Labda Bibi atakuja kujionyesha kwetu hapa hapa." Hata hivyo walijitahidi kutolea huzuni ile kama sadaka. Wakaumalizia usiku wote gerezani!

Kesho yake Fransis alikuwa na huzuni kubwa karibu atokwe machozi. Akasema, "Hakika Bibi yetu amepata uchungu sana sababu hatukufika huko shimo la Iria. Naogopa hatajionyesha kwetu tena."

Lusia akamfariki akisema; " Sijui. Lakini natumaini atarudi". Fransis akapata tena tumaini. Akasema: "Afadhali, maana namkumbuka sana."
Yasinta alikuwa akilia bado kwa uchungu akikumbuka familia yake hasa mama yao. Fransis akachukua jukumu la kumbembeleza akimwambia hata kama itatokea wasiwaone tena wazazi na ndugu zao wavumilie tu na watolee jambo hilo kwa wongofu wa wakosefu.

Watoto waliendelea kutishwa vikali. Hata hivyo kukawa na wasiwasi kuwa watu waliokusanyika kule Fatima wangeweza kusababisha fujo kwa kuwa walishafahamu kuwa watoto wametekwa, wakuu wa serikali wakaogopa. Wakawafanyia tena mahojiano ya mwisho halafu wakawaachia huru warudi makwao.

Walipotoka gerezani Lusia, Fransis na ndugu yake aitwaye Johani walikwenda kuchunga kondoo eneo liitwalo Valinhos. Wakiwa katika eneo hilo walihisi jambo lisilo la kawaida. Wakadhani labda Bibi anataka kuwatokea. Kwa kuwa Yasinta hakuwepo, walimwomba Johani akamuite. Johani akawa mbishi kidogo. Lusia alikuwa na sarafu chache zisizo na thamani kubwa. Akampa ili akubali kwenda. Johani akazisukumiza mfukoni kisha akaenda kumuita Yasinta.

Wakati ule ule Lusia na Fransis waliona mng'aro wa mwanga. Punde Yasinta naye akawasili. Muda mfupi baada ya Yasinta kufika watoto wakamuona Bibi amesimama juu ya mti.

Lusia akamuuliza "Unataka nifanye nini?" Bibi akajibu: "Nataka muendelee kwenda kule Shimo la Iria tarehe 13 ya kila mwezi, na muendelee kusali Rozari kila siku. Katika mwezi wa mwisho nitafanya muujiza kusudi watu wote wasadiki."

Watu waliokuwa wakienda kule shimo la Iria walikuwa wakitoa fedha (sadaka). Lusia akamuuliza yule Bibi wazifanyie nini hizo fedha? Bibi akamjibu kuwa watumie zile fedha kutengeneza majukwaa mawili yanayobebeka (portable stands). Majukwaa hayo yauzwe na fedha itakayopatikana itumike kuandaa sikukuu ya Malkia wa Rozari. Na fedha itakayobaki itumike kujenga kanisa mahali pale.

Lusia alimuomba Bibi awaponye wagonjwa. Bibi akamwambia wapo wagonjwa atakaowaponyesha wakati fulani mwaka huo huo.

Bibi akaonyesha sura ya huzuni sana halafu akasema: "Salini, na tena salini sana, toleeni sadaka kwa ajili ya wakosefu. Roho nyingi sana zinakwenda motoni kwa sababu hakuna mtu wa kuziombea, wala wa kutolea sadaka kwa ajili yao."

Akiisha kusema hayo akapaa kama desturi yake.

Awatokea kwa mara ya tano

Habari za Bibi kuwatokea watoto hawa zilienea sana. Watu wakatoka pande mbalimbali kwenda kuwaona watoto au kusali pale Shimo la Iria.

Watoto nao waliongeza bidii ya kusali na kutolea sadaka. Walianza hata kujitesa kwa kujifunga kamba viunoni nayo ikabana kuwatia maumivu.

Tarehe 13 Septemba ikawadia. Makundi makubwa ya watu yalikuwa yamefika Fatima. Wengi wakajipanga barabarani kuelekea shimo la Iria. Wengine walitaka tu kuwaona watoto lakini wengi walitaka kuwakabidhi watoto maombi yao wayapeleke kwa bibi. Huyu atakuwa anamwombea mwanae kiwete na yule labda anaomba mgonjwa wake kipofu aponywe. Sauti itasikika huku ya mama akiomba mumewe aliye vitani arudi salama au mwingine atalalamika kifua kinampa maumivu anaomba Bibi amponye. Alimradi kulikuwepo maombi ya aina aina, wote wakitaka watoto wayafikishe kwa Bibi.

Msongamano wa watu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba watoto walipita kwa shida hadi ikabidi wanaume mabaunsa wajitokeze kupangua watu ili njia ipatikane na watoto wapite kwenda shimo la Iria kama walivyokuwa wameelekezwa na Bibi.

Hatimaye watoto walifika shimo la Iria. Wakakaa pale kwenye mti pamoja na makusanyiko ya watu wakaanza kusali rozari. Muda si muda watoto wakaona mg'aro wa mwanga na Bibi akafika juu ya ule mti. Bibi akasema,

"Endeleeni tu kusali rozari kusudi vita ifikie mwisho. Katika mwezi Oktoba atakuja Bibi...! . Mungu ameridhishwa na sadaka zenu. Hataki muendelee kulala na kamba zenu viunoni, mtazivaa wakati wa mchana tu."

Lusia alimwambia amepewa mambo mengi ya kuomba kuponyesha wagonjwa, bubu, viziwi nk. Bibi akamjibu kuwa wengine atawaponyesha lakini wengine hatawaponyesha.Akarudia kusema kuwa mwezi Oktoba atafanya muujiza kusudi wote waweze kusadiki. Baada ya hapo kama ilivyo desturi akaanza kupaa hadi akatoweka.

Tokea la sita na la mwisho

Tarehe 13 Oktoba ilifika. Hii ni tarehe ambayo Bibi alisema atafanya muujiza. Kama kawaida taarifa za Bibi kutokea zilishasambaa mno na watu walikuwa wengi sana.

Watoto waliamka na kujiandaa kwa miadi ya Bibi. Hii pia ndio siku Bibi alipanga muujiza ili watu waamini. Watoto wakaaamka mapema ili wakwepe msururu wa watu.

Baada ya kufika yakatokea matukio kadhaa yenye miujiza mikubwa, na kwa hakika tokeo hili lilikuwa na miujiza ya kiwango cha kustaajabisha mnooo kuliko matokeo yaliyotangulia.

Kwanza baada ya Bibi kutokea, alionekana Mt. Yosefu akiwa pembeni ya jua akiwa na Mtoto Yesu na Bikira Maria wa Rozari. Bikira Maria alionekana amevaa nguo nyeupe na joho la bluu. Mt. Yosefu pia alivaa kanzu nyeupe na akaonekana akifanya ishara ya msalaba kubariki dunia.

Bikira Maria akaonekana pia anachomwa kwa panga za mateso kwenye moyo wake. 

Bibi akawaambia watoto kwamba anataka kikanisa (Chapel) kijengwe eneo lile kwa heshima yake. Kisha akajitambulisharasmi kwa wale watoto kuwa yeye ni Malkia wa Rozari. Akawaagiza waendelee kusali rozari kila siku.

Lusia alipomwomba Malkia wa Rozari aponyeshe wagonjwa na kuwaongoa wakosefu Malkia alijibu kuwa baadhi watapona lakini wengine hapana. Alisema watu warekebishe kwanza hali zao na kuomba msamaha kwa dhambi zao. Wasiendelee kumkosea Bwana wetu maana ameshakosewa sana.

Muujiza mkubwa na wa kutisha

Malkia wa Rozari akafumbua mikono yake ndipo muujiza wa jua ukaanza kutokea. Mwanga kutoka kwa Malkia wa Rozari ukawa unalielekea jua. Lusia akasema kwa mshangao: "Angalieni jua!"

Watu zaidi ya elfu 70 walikuwa wakishuhudia muujiza huu. Jua lilionekana kama sahani kubwa ya fedha (silver) likin'gaa kuliko namna yoyote iliyowahi kutokea lakini ajabu ni kuwa halikuumiza macho ya waliolitazama. Baada ya muda mfupi jua likaanza kucheza kwa mtikisiko likawa kama linacheza densi. Hali hii ilidumu kwa kitambo halafu likabadilika tena na kuanza kuzunguka kama tairi. Wakati likifanya hivi lilitoa miali myekundu ya moto huko angani na miali hii ilitoa mwanga uliofika hadi chini kwenye miti na hadi kuwafikia watu waliokuwepo pale.

Kisha jua likabadilika na kuwa kama duara la moto na likaanza kuzunguka kwa kasi. Kisha jua likaonekana kama tufe la moto likiwasogelea watu kwa kasi. Umati ukapata hofu. 

Baada ya hapo jua likaanza kurudi mahali pake kwa mwendo wa zigzag. Halafu likatulia kabisa.

Kabla ya muujiza huo mvua ilikuwa imenyesha kubwa na nguo za watu kulowana. Ila wakati wa muujiza huo nguo za watu wote zilikauka. Muujiza ulishuhudiwa na watu waliokuwa hadi umbali wa kilometa 40 kutoka eneo la tokeo.

Huu ni muujiza aliokuwa amehaidi Malkia wa Rozari ili watu waamini kuwa amewatokea watoto wale. Basi siku hii ya tarehe 13 Oktoba 1917 ikawa pia ndio mwisho wa matokeo ya Maria kwa wale watoto. Alikuwa amewatokea kwa mara sita. Zote ikiwa ni tarehe 13 ya kila mwezi kuanzia mwezi Mei 1917, isipokuwa mwezi Agosti ambao aliwatokea tarehe tofauti kwa kuwa siku ya tarehe 13 watoto walikuwa gerezani.

Hatimaye kanisa laanza kutambua matokeo ya Fatima baada ya uchunguzi mkali wa muda mrefu.

Baada ya tokeo hili la mwisho mambo hayakuwa mepesi kwa watoto. Walihojiwa sana sana na kanisa na serikali. Baada ya uchunguzi mkali wa kanisa kwa miaka 13, hatimaye Oktoba 1930 Askofu wa Leira-Fatima alitangaza rasmi kuwa kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na kwa kusikiliza ushauri wa tume ya kichungaji iliyofuatilia uchunguzi wa matukio hayo na kwa kujiweka chini ya ulinzi wa Mama Maria mtakatifu sana na kwa ushauri wa mapadre wa jimbo anatangaza rasmi kuwa matokeo waliyopata watoto wachungaji yanafaa kuaminiwa katika jimbo hilo na akaruhusu rasmi ibada na heshima kwa Bibi yetu wa Fatima.

Baada ya hapo mapapa kadhaa walitambua na kukubali habari za Fatima. Papa Pius wa XI kwa mfano alitoa rehema ya muda kwa wale ambao wangetembelea kanisa lililojengwa Fatima kisha wakasali kwa nia za Baba Mtakatifu.
Pia Papa Pius XII mwaka 1940 alizungumzia matokeo ya Fatima katika andiko rasmi la kipapa kwa mara ya kwanza. Mapapa waliofuata waliendeleza kutambua na kuenzi matokeo hayo na mwaka 1982 Papa Yohane Paulo II alitamka rasmi kwamba ujumbe wa Fatima una misingi yake katika Biblia.

Siri 3 za Fatima ni zipi?

Pamoja na ukweli kuwa kutokea kwa Bikira Maria kulileta hali ya watu wengi kuvutiwa na matukio hayo, bado wengi wao walikuwa na hamasa ya kujua siri walizoambiwa wale watoto. Watoto walibaki waaminifu wakitunza yale waliyokatazwa kusema. Hata hivyo baada ya kitambo kirefu Lucia aliruhusiwa kuweka wazi siri mbili walizoonyeshwa.Siri hizi walionyeshwa katika tukio la tarehe 13 Julai 1917. 

Siri ya kwanza ilikuwa ni siri ambayo Mama Maria aliwaonyesha watoto siku ile mwezi Julai miale ya mwanga toka mikononi mwake ilipofunua ardhi watoto wakaogopa sana na kupiga kelele. Aliwawezesha kupaona waziwazi motoni kwa macho yao ya nyama. Aliwafunulia Jehanamu ya moto wa milele wakaona kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko.

Huko waliona mashetani yaliyotumbukia humo, na wakaona roho za watu zinazofanana na makaa ya moto. Roho hizo zilikuwa zikipeperuka ndani ya moto huo katika hali ya hasira na chuki. Zilitoa vilio vya hofu na kutweta kwa mateso na kukata tamaa.

Bikira Maria akawaambia watoto, "Sasa mmeona moto wa milele ambamo roho za wakosefu maskini huenda. Kusudi wakosefu waokolewe, Mungu anataka patengenezwe duniani ibada kwa Moyo wangu Safi. Iwapo hayo niliyowaambia yatatimizwa roho nyingi zitaokolewa.Tena mnaposali Rozari, baada ya kila fumbo mtasema maneno haya: Ee Yesu wangu, utusamehe, utuepushe moto wa milele; peleka roho zote mbinguni, hasa zilizo katika hatari kubwa."

Kwa hiyo siri ya kwanza ilikuwa hasa kuelezwa nia ya Mungu kuanzisha ibada kwa Moyo wa Maria usio na doa kwa ajili ya wongofu wa wakosefu na kuipatia dunia amani.

Siri ya pili

Itakumbukwa kwamba wakati Bikira Maria anawatokea watoto wale, dunia ilikuwa inapitia kipindi kigumu sana cha vita ya kwanza ya dunia. Watu wengi walikuwa wameuawa na hakukuwa tena na amani. Wengi waliamini kwamba ule ndiyo ulikuwa mwisho wa dunia, na kwa hakika walikata tamaa. Katika matokeo yake kwa watoto wale, Bikira Maria daima aliwasisitiza wasali rozali na kujitesa kama sadaka ili vita ile imalizike. Maana yake ni kwamba bila Rozali huenda vita ile isingekwisha na kweli ingeweza kuwa mwisho wa dunia.

Hivyo siri ya pili ilikuwa ni unabii wa kuisha kwa vita ya kwanza ya dunia na kuanza kwa vita ya pili ya dunia. Bikira Maria aliwaambia kuwa vita hiyo ya kwanza ya dunia ilikuwa inakaribia kuisha lakini kama watu hawataacha kumkosea Mungu kutakuwepo na vita mbaya zaidi wakati wa upapa wa Papa Pius XI.

Pia alitoa unabii kwamba kanisa na Baba Mtakatifu wangepata mateso makali kwa sababu dhambi zilizidi duniani.

Na ili kukwepa adhabu, Mama Maria angerudi wakati mwingine kuomba Urusi iwekwe wakfu kwa Moyo Safi wa Maria, na kuomba Komunio ya malipizi kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi. Kama maombi ya Mama yatasikilizwa, Urusi ingeongoka na kungekuwepo amani.

Bikira Maria akawahakikishia watoto wale kwamba mwisho wa yote Moyo Safi wa Imakulata utashinda na Urusi itawekwa wakfu kwake na Urusi itaongoka, na kisha kitafuata kipindi cha amani duniani.

Siri ya tatu

Siri ya tatu ya Fatima ni kubwa zaidi na imekuwa jambo la ubishani mkubwa kwa baadhi ya watu. Tofauti na siri mbili zilizotangulia ambapo Lusia aliruhusiwa na Maria kuzitoa, siri ya tatu haikuwa hivyo moja kwa moja.

Kilichotokea ni kuwa Lusia aliugua sana. Askofu wake akijua kuwa bado kuna siri haijafumbuliwa, alimwagiza Lusia aiandike siri hiyo ili endapo atakufa basi siri hiyo iwepo. Lusia alisita sana kufanya hivyo lakini kwa utii mtakatifu na akijua Askofu yule ni wakili wa Kristu alikubali kuiandika.
Siri hii iliwekwa katika bahasha iliyofungwa kwa lakiri (seal) na baadaye bahasha ile ilipelekwa kuhifadhiwa Vatican yaliko makao makuu ya kanisa.

Mwaka 1960, Papa Yohane XXIII aliifungua bahasha ile na kuisoma hiyo siri. Kwa hekima yake ya kichungaji na baada ya kupata ushauri wa kardinali Ottavian akaona sio muda muafaka wa kuifumbua. Papa akaiweka katika bahasha mpya akafunga tena na kuirudisha katika chumba cha nyaraka za siri. Alipokuja Papa Paulo VI naye akaona hati ile ibakie siri vile vile.

Hatimaye siri hii ilifumbuliwa wakati wa upapa wa Papa Yohane Paulo II, na iliwekwa wazi mwaka 2000.

Siri hii ilikuwa ni utabiri wa kupigwa risasi kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, pamoja na matukio ya kutekwa na hata kuuawa kwa maaskofu na mapadri na watawa na wafuasi mbalimbali wa Kristo kokote duniani kama malipizi kwa sababu ya maasi yanayoendelea duniani.

Ikumbukwe kwamba Papa Yohane Paulo wa Pili alikuja kupigwa risasi tarehe 13 Mei 1981, siku na tarehe hiyohiyo ambayo kanisa lilikuwa linaadhimisha miaka 64 kamili tangu tokeo la kwanza la Bikira Maria huko Fatima. Aidha, tukio hili lilitokea mwaka mmoja kamili kabisa (kwa tarehe na mwezi) kabla Papa huyu huyu hajatangaza rasmi kanisa kuyatambua matokeo yote ya Bikira Maria huko Fatima, tangazo alilolitoa tarehe 13 Mei 1982.

Katika siri hii, watoto waliona malaika amekaa kushoto kwa Bikira Maria akiwa na upanga unaotoa miali ya moto akiwa ameushikilia kwa mkono wake wa kushoto. Upanga huo ulitoa miale ya moto kana kwamba ingeunguza dunia yote lakini miale hiyo ilizima ilipokutana na mwanga wa ajabu uliotoka kwa mama Maria. Malaika akatoa sauti kubwa akisema "Malipizi, malipizi, malipizi." 

Watoto waliona mwanga ambao ni Mungu mwenyewe! Walimuona Mungu.

Kisha watoto waliona mtu ambaye walidhania ni askofu. Kisha wakaona mwingine mwenye mavazi meupe ambaye walimtambua kuwa ni Papa. Wakaona maaskofu na mapadre, watawa wa kike na kiume wakipanda mlima mkali. Juu ya mlima kulikuwepo Msalaba mkubwa. Kabla ya kuufikia msalaba huu Papa alipitia jiji kubwa lililoharibiwa vibaya na lilikuwa kwenye mateso na maumivu makali.

Papa akawa anasali kwa ajili ya roho za maiti aliopishana nazo. Alipofika msalabani pale juu ya mlima akapiga magoti chini ya msalaba. Kisha akavamiwa na kundi la wanajeshi waliomuua kwa risasi na mishale. Na kwa namna hiyo hiyo wakauawa maaskofu, mapadre, watawa na watu wengine wa aina tofauti tofauti. Katika kila upande wa Msalaba walikuwepo malaika waliokusanya damu ya mashahidi waliouwawa na wakainyunyizia kwa roho zilizokuwa zikijitahidi kumuendea Mungu.

Kwa ufupi kanisa linaamini maono ya siri hizi tatu ni vita inayopiganwa na wakana Mungu dhidi ya Kanisa. Ujumbe muhimu ni kwamba wote tufanye toba.

Kifo cha Fransis

Fransis aliyezaliwa June 11, 1908 ndiye aliyekuwa wa kwanza kufariki kati ya watoto wale. Ikumbukwe kwamba hata walipokuwa gerezani mwaka mmoja uliotangulia yeye alikuwa akitamani kufa mapema ili awahi kwenda mbinguni kwa Bibi.

Mwaka 1918 huko Ulaya uliibuka ugonjwa wa homa kali ya mafua. Ugonjwa huu uliwakumba watu wengi na Fransis naye alikumbwa na ugonjwa huu. Ugonjwa ulikuwa mkali kwa Fransis kiasi kwamba alilala kitandani muda mrefu. Lusia alikuwa akienda kumjulia hali na mara nyingi alimuuliza ikiwa maumivu yalikuwa makali. Fransis alijibu kuwa maumivu ni makali sana lakini hajali kitu kwa kuwa anateseka ili kumtuliza Bwana Yesu. Akazoea kusema; "Bado kidogo nitakwenda mbinguni". Hapo alikuwa ni mtoto mwenye umri wa miaka 10 tu.

Lusia alimwambia akifika mbinguni asisahau kuwaombea wakosefu, yeye Lusia, Yasinta na Baba Mtakatifu. Fransis akamwambia sawa lakini huenda nikasahau. Kazi yangu kubwa huko itakuwa kumtuliza Bwana Yesu!

Siku moja asubuhi Fransis alizidiwa sana. Lusia akaitwa aende kumuona mgonjwa. Lusia alipofika Fransis akaomba ndugu na mama yake watoke nje wabaki yeye na Lusia tu. Walipotoka chumbani Fransis akamwambia Lusia kuwa anataka kuungama ili apokee Komunio Takatifu kisha afe. Akamwambia Lusia amsaidie kukumbuka dhambi alizomwona akitenda.
Yasinta akampa Lusia orodha ya dhambi ambazo Fransis anatakiwa kuungama. Lusia alipomweleza Fransis, kijana akamuambia kuwa hizo alishaziungama kitambo lakini akasema ataziungama tena. Akafanya sala ya kutubu na kumuomba Lusia pia amuombee msamaha kwa Yesu.

Baada ya hapo alimwomba Lusia amuite paroko. Paroko alipofika alimpatia maungamo na kumwambia kuwa angempelekea Komunio Takatifu kesho yake. Kesho yake paroko alitimiza ahadi. Akampelekea Ekaristi. Akiisha kukomunika alimwambia Yasinta:- "Mimi nina heri zaidi kushinda wewe. Yesu mfichama yuko ndani yangu na pili naenda zangu mbinguni."

Baada ya Fransis kupokea Ekaristi, Lusia na Yasinta walishinda kando ya kitanda chake. Fransis alikuwa ameishiwa nguvu ya kusali hivyo akawaomba Lusia na Yasinta wamsalie rozari.

Usiku ulipowadia Lusia alitakiwa kurudi nyumbani. Akamwambia Fransis, "Kwa heri Fransis! Ikiwa utasafiri usiku huu kwenda mbinguni ukishafika huko usinisahau. Unasikia?"

"Hapana sitakusahau, usiwe na shaka.". Akajibu Fransis kisha akaukamata kwa nguvu mkono wa kulia wa Lusia huku macho yake yamejaa machozi. Lusia pia akabubujikwa machozi.

Fransis alikuwa ameishiwa nguvu kabisa. Lusia akamwambia Fransis taratibu; "kwa heri mpaka tutakapoonana mbinguni."

Lusia akaondoka.

Mama yake Fransis akabaki chumbani. Ilikuwa usiku wa tarehe 4/4/1919 wakati Fransis alipomuita mama yake na kumwambia: " Mama angalia ule mwanga mzuri karibu na mlango." Ilikuwa kama saa kumi hivi za usiku (alfajiri?), Francis akatulia tena. Akamuomba radhi mama yake kwa makosa aliyowahi kumtendea. Ikaonekana kama maumivu yamekwisha. Uso wake ukang'aa kwa mwanga wa kimalaika. Roho yake ikapaa mbinguni mikononi mwa Mama Maria. Huo ndio ukawa mwisho wa Fransis hapa duniani.

Lusia anasema kwamba uchungu wa kumkosa Fransis ulikuwa kwake kama mwiba uliopita moyoni.

Kifo cha Yasinta

Kama ilivyokuwa kwa Francis, Yasinta naye aliugua ugonjwa ule wa mafua makali. Lakini Yasinta aliteseka kwa kitambo kirefu zaidi huku akimtolea Mungu mateso na maumivu yake kama sadaka yake kwa ajili ya wakosefu.

Lusia alikuwa akienda kumsalimu mara kwa mara. Siku moja Yasinta alimwambia Lusia, "Nenda kwa Yesu mfichama (Ekaristi takatifu) umwambie kuwa mimi nampenda sana. Umsisitizie mpaka ajue kwamba ni kweli kabisa ninampenda, basi tu".

Wakati akiwa mgonjwa kitandani, alikuwa akijinyima chakula ili atoe sadaka kwa ajili ya wakosefu. Mama yake akamsisitiza ale lakini yeye alikataa. Siku moja Lusia akamwambia Yasinta kuwa anapaswa kutii anapoambiwa na mama yake ale. Yasinta alihuzunika sana alipotambua kwamba amekosa utii kwa mam. Kuanzia siku hiyo hakukataa chakula bali alitolea uchungu wake wa kukosa fursa ya kujinyima chakula kama sadaka. Kitendo cha kula bila kujinyima kilimfanya ajisikie kinyaa, lakini hakuonyesha usoni zaidi ya kutolea kimya kimya kinyaa kile kuwa sadaka yake.

Siku moja wakati akiwa katika ugonjwa wake na wakati huo Fransis akiwa bado hajafariki, Mama Maria alimtokea. Akamwambia kuwa angerudi tena siku za karibuni kumchukua Francis, na kwamba yeye Yasinta ataendelea kupata maumivu mengi na makubwa kwa ajili ya wongofu wa wakosefu na malipizi ya dhambi zinazouumiza Moyo Safi wa Maria na kwa ajili ya kumpendeza Yesu.

Yasinta alimwambia Lusia kuwa Bikira Maria alimwambia pia kuwa atahamishiwa kwenye hospitali nyingine, taarifa ambayo ilimuumiza sana hasa kwa kujua atakuwa mbali na Lusia. Wakati huo huo Francis alikuwa pia katika hatua za mwisho kabla ya kifo chake. Yasinta akamtumia ujumbe wa buriani akimwambia Francis atakapokufa afikishe salamu za upendo kwa Yesu na Maria. Pia awaarifu kuwa yuko tayari kuteswa kadiri wapendavyo kwa ajili ya wongofu wa wakosefu na malipizi ya dhambi. Muda mfupi baadae ndipo Francis aliaga dunia, jambo lililomtia uchungu mkubwa Yasinta.

Utabiri wa Mama Maria ulitimia. Yasinta alipaswa kuhamishwa hospitali kwenda hospitali ya mbali zaidi na nyumbani alikaa katika hospitali hii kwa muda kisha akatakiwa kuhamia hospitali ya Lisbon. Mama Maria alimwarifu kabla kuwa akienda Lisbon hatawaona tena wazazi wake wala 
Lusia lakini mama Maria akamwambia asiogope yeye atakwenda kumchukua ampeleke mbinguni muda ukifika.

Yasinta aliteseka vikali sana kuhusu upweke uliokuwa ukimsubiria. Alimwambia Lusia, sitakuona tena wala hutaweza kunitembelea tena. Uniombee kwa sababu naenda kufa. Sitawaona kaka zangu wala baba yangu. Nitafariki huko peke yangu. Lusia alijaribu kumshauri asiyawaze hayo lakini Yasinta akasema anayawaza ili apate uchungu na mateso ampendeze Bwana Yesu. Cha ajabu ni kwamba huyu Yasinta aliyeugua kwa imani kubwa kiasi hiki alikuwa na umri wa takribani miaka 8 tu. Tazama ajabu ya Mungu katika imani ya mtoto mdogo kiasi hiki !!!! Katika maumivu hayo mara kwa mara Yasinta alishika Msalaba na kuubusu akisema Yesu nakupenda.

Mama yake alipoonekana kuumia sana kwa mateso ya mwanae, Yasinta alimfariji kuwa asihangaike maana anakwenda mbinguni.

Siku ya kuhamia hospitali ya Lisbon ikifika. Ilikuwa uchungu mkubwa kwake kutoa mkono wa buriani kwa wapendwa wake. Alimkumbatia Lusia shingoni kwa kitambo kirefu akihema huku akisema, "Lusia hatutaonana tena. Uniombee mpaka siku yangu ya kwenda mbinguni. Ufanye sadaka nyingi kwa ajili ya wakosefu."

Alisafiri kwenda Lisbon akiwaacha wapendwa wake nyuma. Akiwa hospitali huko Lisbon alimtumia Lusia ujumbe kuwa Mama Maria alimtokea tena na kumtaarifu kuhusu siku na saa ya kufa.

Tarehe 19 February 1920, Yasinta alimwomba padre wa pale hospitalini ampatie Komunyo Takatifu na mpako wa Wagonjwa kwa kuwa angekufa usiku utakaofuata. Kweli usiku wa tarehe 20 February 1920 Yasinta akiwa na umri wa miaka 9 alifariki akiwa peke yake kama ilivyotabiriwa.

Ugumu wa kuwatangaza watoto hawa kuwa watakatifu

Kabla ya kueleza kwa ufupi sana kuhusu kifo cha Lusia kwanza tuone kwamba haikuwa rahisi kuwatangaza watoto hawa kuwa watakatifu kwa utaratibu wa kawaida wa Kanisa katoliki. Sababu kubwa ya kanisa kutotangaza watoto wadogo watakatifu ni ukweli kwamba kunakuwepo na mashaka ikiwa watoto wadogo wanatambua fadhila walizo nazo ili waweze kuwekwa kama kielelezo kwa wengine.

Hoja hii ilichelewesha kwa kiasi kikubwa mchakato wa kuwatangaza watakatifu,kiasi kwamba walikuja kutangazwa watakatifu zaidi ya miaka 80 baada ya kufariki.

Mwaka 1979 baraza la kutangaza watakatifu (congregation for the causes of Saints) liliitisha mkutano ambapo kulikuwepo makardinali, maaskofu na wanateolojia kujadili endapo inawezekana watoto kuonyesha ushujaa wa fadhila kwa kiwango cha kutangazwa watakatifu. Baada ya mjadala wa kina ilikubalika kuwa kama ambavyo watoto wanaweza kuonyesha vipaji vya pekee mara chache kwenye mambo ya kidunia kama vile muziki au hesabu, inawezekana pia kwa nguvu zisizo za kimaumbile (supernatural way) watoto kuwa na maelekeo makubwa ya kiroho.

Mei 13, 2000 watoto hawa Yasinta na Fransis waliotangazwa watakatifu. Yasinta ni Mtakatifu mwenye umri mdogo zaidi kutangazwa Mtakatifu asiyekuwa shahidi.

Kufariki kwa Sr. Lusia

Lusia aliishi muda mrefu zaidi. Alizaliwa mwaka 1907 na kufariki Februari 13, 2005 akiwa na miaka 98. Ingawa mwezi ni tofauti, lakini tarehe ya kifo chake ni ile ile 13 ya matokeo ya Bikira Maria kule Fatima. Tena kifo chake kilitokea takribani mwezi mmoja na nusu tu kabla ya kifo cha Papa Yohane Paulo II, Papa ambaye Mama Maria alionesha Lucia siri kwamba angepigwa risasi, papa ambaye ndiye aliyerasimisha zaidi matokeo na miujiza ya Fatima katika kanisa, na papa ambaye ndiye aliyewatangaza Francis na Yasinta kuwa watakatifu.

Katika maisha yake alijiunga na utawa wa wakarmeli. Kutokana na umri mkubwa na ugonjwa, inasemekana Sr. Lusia alikuwa amepoteza uwezo wake wa kuona na kusikia wakati wa kifo chake. Alipokufa nchi yake ya Ureno ilitangaza maombolezo ya kitaifa tarehe 15 Februari 2005.

Sr. Lusia anatarajiwa kutangazwa Mtakatifu kesho tarehe 13 Mei 2017 na Baba mtakatifu Fransis wakati wa maadhimisho ya miaka 100 tangu tokeo la kwanza la Bibi yetu wa Rozali Bikira Maria wa Fatima.

 Bikira Maria Malkia wa Rozali - Utuombee .
12 May 2017 ·