Rozari takatifu ni sala kutoka Mbinguni. Bikira Maria alimkabidhi Mtakatifu Dominiki mwaka 1214 katika msitu wa Toulouse ambapo alienda kwa mafungo. Huko alisali usiku na mchana bila kula wala kunywa akifanya toba na malipizi. Usiku wa siku ya tatu alizimia ndipo Bikira Maria alimtokea akiwa amefuatana na malaika watatu na alimkabidhi Mtakatifu Dominiki Rozari Takatifu, kisha akamfundisha namna ya kuisali. Alimfundisha matendo ya furaha, uchungu na utukufu kwa maana ya kusali tasbihi tatu ambazo ni Rozari moja. Papa Yohane Paulo wa II mwaka 2002 aliongeza matendo ya mwanga ambapo sasa tunasali tasbihi nne ambazo ni Rozari moja. 

MUUNDO WA ROZARI TAKATIFU: 
KANUNI YA IMANI: “Nasadiki kwa Mungu…..”
(Heb.11:6) Yeyote ajaye kwa Mungu lazima awe na imani. Anayempenda Mungu kwanza anamwamini na kwa kadri ya imani hiyo sala zake zitakubaliwa, ndivyo itakavyokuwa na nguvu na ndivyo itakavyomtukuza Mungu. 
 
BABA YETU “SALA YA BWANA”: 
Ni sala aliyofundisha Mungu. Mitume walimwomba Yesu awafundishe namna ya kusali naye akawafundisha kusali sala hii ya Baba yetu. (Mt.6:9-13)

SALAMU MARIA(MAAMKIO YA MALAIKA):
Sala hii ni mjumuisho wa maamkio ya malaika Gabrieli, maneno ya Elizabeth alipojazwa Roho Mtakatifu baada ya maamkio ya Bikira Maria kwa Elizabeth na sala ya Kanisa Takatifu. (Lk 1:28: lk1:42) 

ATUKUZWE BABA…
Hii ni sala ya kutukuza utatu mtakatifu (Ufu4:10-11).

EE YESU MWEMA..(SALA YA FATIMA)
Sala aliyoitoa Bikira Maria kule Fatima tarehe 13/07/1971 kuomba Yesu atuepushe na moto wa Jehanamu. 

MATENDO YA ROZARI TAKATIFU: 
Matendo ya Furaha (Jumatatu na Jumamosi)
Matendo ya Uchungu (Jumanne na Ijumaa)
Matendo ya Utukufu (Jumatano na Jumapili)
Matendo ya Mwanga (Alhamisi)

Kusali Rozari takatifu ni kutafakari Maisha, mateso, kifo na utukufu wa mkombozi wetu Yesu Kristo. Yote hayo yapo kwenye Biblia Takatifu. 
Rozari siyo mkusanyiko wa baba yetu na salamu maria nyingi, bali ni muhtasari mtakatifu wa mafumbo ya maisha, kifo, mateso na utukufu wa Yesu na Maria. 
Msomi Kajetani anasema…..”kuacha kusali sala ya Baba yetu na Salamu Maria ni kudondoka katika chambo cha ndoto za shetani. 

Sala hii ni kinga, nguvu na usalama wa mioyo yetuu. Bikira Maria alimweleza Mtakatifu Getruda kuwa hapajatokea binadamu yeyote aliyeweza kumtungia kitu chochote kilicho kizuri kama Salamu Maria”. 
Hapatakuwepo na maamkio yoyote yenye thamani katika Moyo wangu kama uzuri na heshima iliyopo katika maneno yaliyotoka kwa Mungu Baba. 

Rozari Takatifu ina sehemu kuu mbili ambazo ni kutafakari na kusema kwa sauti. Tafakari ni kuwaza yale mafumbo makuu ya maisha, mateso, kifo na utukufu wa Yesu Kristo na Mama Bikira Maria; kusema kwa sauti inaunganisha kusali mafumbo yote ishirini kila fumbo likitanguliwa na Baba yetu moja na salamu maria kumi, atukuzwe baba na Ee Yesu mwema…..