Rozari Hai si Ibada mpya, hapana! Bali ni ibada ile ile aliyohubiri Mt.Dominiki na kusisitizwa sana na Bikira Maria katika matukio yake mbali mbali. Rozari Hai ni njia tu ya kusali Rozari nzima(Tasbihi nne) kwa njia ya kushirikiana watu 15/20 pamoja, japokuwa hawakai pamoja. Watu hawa 15/20 wanashirikiana kusali Rozari nzima, kwa jinsi kila mmoja wa hawa watu 15/20 anasali kumi moja tu na kutafakari fumbo linalohusika na kumi hilo.
Hivyo watu watano wa kwanza wanagawana mafumbo matano ya Furaha, watano wanaofuata wanagawana mafumbo matano ya mwanga, watano wanaofuata wanagawana mafumbo matano ya Uchungu na wa mwisho watano wanagawana mafumbo matano ya Utukufu. Hivyo kila mmoja katika hawa watu 20 akisali kumi lake moja alilogawiwa na Makao makuu, anapata Neema na mastahili ya Rozari nzima (Tasbihi nne-mafumbo yote 20 ambayo ndiyo rozari moja Kamili).
Kila mwanachama aliyejiunga na Rozari hai, anatakiwa awe mwaminifu kusali kumi lake kila siku kwa maisha yake yote, vinginevyo Rozari hiyo haiwezi kuwa hai tena.
Mtu akitaka anaweza kuchukua zaidi ya kumi moja, mradi awe tayari kuyasali makumi hayo kwa uaminifu kila siku. Hivyo usichukue zaidi ya uwezo wako wa kuyasali.
(Faraja ya Uponyaji wa Moyo wa Maria; Tone kwa Tone Muongo kwa Muongo)