Rehema kamaili inakirimiwa kwa kusali tendo moja la mafumbo matano, usalipo Kanisani katika sala ya halaiki, usalipo katika familia, katika nyumba za kitawa au katika chama cha kitume wasali kwa sauti na kwa kupokezana huku wakiwaza na kuyatafakari Mafumbo hayo. Pia usalipo Rozari Takatifu mbele ya Ekaristi Takatifu (ndani ya kikanisa cha kuabudia au mbele ya Tabernakulo au mbele ya Yesu wa Ekaristi aliyewekwa kwa Ibada maalum kama vile mkesha n.k)lazima kusali Rozari hiyo kukujiunganisha na Tabernakulo zote Dunia kwa Sala ya Rozari hiyo.Katika Rozari ya halaiki ni lazima kutaja mafumbo kwa sauti kadri ya utaratibu wa mahali (Masharti ya kupata Rehema kwa sala ya Rozari takatifu yazingatiwe). Rehema pungufu inapatikana kwa Rozari iliyosaliwa kwa namna nyingine.

Ili kupata Rehema kamili ni lazima kutimza masharti yanayoendana na Rehema husika ambayo ni kupata Sakrament ya ungamo, kupokea ekaristi takatifu na kusali kwa ajili ya nia za Papa. (Kusali kwa ajili ya nia za Papa-unaweza kusali Baba yetu moja, Salamu Maria moja na Atukuzwe Baba moja, ila unaweza kuongeza sala nyingine).

Kila mara tunaposali litania ya Bikira Maria na kuzitafakari, tunapata Rehema za siku 300 (Papa Pius VII, 30/09/1817).

*Ndugu zangu tunapoendelea na mwezi wa Maria ningependa tutafakari juu ya kitu muhimu sana katika maisha yetu.*

*Kitu hicho ijapokuwa wengi hawakielewi ni cha muhimu sana hasa kwa siku ya leo na kipindi hiki kwa ujumla, ambacho yeyote atakayekisoma na kukishika kamwe hataukosa Ufakme wa mbinguni.*

_Sasa hebu twendeni pamoja tuelewe nini Maana ya Rehema kamili?_

*REHEMA*

Kwa kifupi tu katika muktadha wa kiimani, neno Rehema laweza kufasiliwa kuwa ni ondoleo la adhabu ambazo Mwanadamu alizistahili ili aweze kuingia mbinguni.

Ni ondoleo la malipizi kwa ajili ya dhambi kubwa na ndogo alizozitenda.

*Aina za Rehema*

Kuna aina mbili za rehema, ambazo ni;

1. Rehema Kamili, na

2. Rehema Pungufu.

*1. REHEMA KAMILI*

Ni maondoleo ya adhabu zote za malipizi ambazo mtu alizistahili, ili aweze kustahilishwa kuingia mbinguni.

*Kwa nini?*

Ikumbukwe kuwa kila dhambi aitendayo mwanadamu, baada ya maungamo sharti lazima ilipiwe, na ndiyo maana Padre hutoa malipizi mbalimbali.

*Je, Malipizi ayatoayo Padre hayatoshi?*

Kumbuka kuwa Padre hutoa malipizi kulingana na jinsi alivyokusikia ukiungama na namna ulivyotaja dhambi hizo.

Aidha, Padre katika ubinadamu wake huenda hataweza kuwa na kipimo halisi kulingana na uzito wa kila dhambi.

Hivyo malipizi akupayo Padre huenda yakatosha kuondoa adhabu zote, au yakapunguza tu.

Mwenyekujua hasa kipimo halisi cha dhambi zako ni Mungu mwenyewe.

Malipizi Mungu huweza kumpa mwanadamu kwa njia mbalimbali kama vile kuruhusu baadhi ya mateso kumpata kama vile magonjwa, kuchukiwa, au kupatwa na jambo lolote linaloweza kumuumiza.

Hayo mateso hayatoki kwa Mungu, lakini Mungu aweza kuruhusu kama sehemu ya malipizi ya dhambi zako, au hata dhambi za watu wengine.

Mt Hyasinta Marto aliombwa na Mama Bikira Maria apokee mateso makali kwa ajili ya wongofu wa wakosefu wengine.

Ikiwa mtu atafikwa na mauti,  akiwa mwenye moyo safi, lakini kabla ya kukamilisha malipizi yake hapa duniani, basi huyo lazima aingie toharani ambako atakamilisha malipizi ya dhambi zake zote.

Huko pia aweza kupunguza muda wa mateso kwa njia ya sala za watu na Watakatifu pia.

*Adhabu ya Toharani*

Ni adhabu kali sana yenye lengo la kufikia kila ovu mtu alilotenda.

Tofauti baina ya adhabu ya Toharani na adhabu ya moto wa milele ni muda tu!

Wakati adhabu ya jehanamu ni ya milele, adahabu ya toharani ni ya muda fulani, ili ikiisha mtu huyo anaingia mbinguni.

Tunapozungumzia Rehema kamili, tunamaanisha ni msamaha au ondoleo la adhabu zote za dhambi alizostahili mtu sababu ya dhambi zilizokwisha ondolewa.

Maana yake mtu mwenye Rehema kamili, akifahuingia mbinguni moja kwa moja.
 
Rehema kamili hutolewa na Kanisa Katoliki kwa kutugawia mastahili ya Yesu Kristo, Bikira Maria na ya Watakatifu.

Rehema kamili inayo masharti yake ambayo Mkristo yeyote akiyafuata huweza kuipokea, kwani Mungu ni mwema, na asiye na upendeo binafsi kwa yeyote.

Yafuatayo ni masharti ya kupata Rehema kamili.

1. *Sharti la kwaza*

Ni kuwa, yeye anayeomba hiyo Rehema Kamili anapaswa kwanza kabisa ajutie dhambi zake zote na kisha aende kuziungama.

Hii ni kwa sababu haiwezekani mkristo apewe Rehema kamili huku akiwa na dhambi, hasa dhambi yoyote ya mauti.

Huwezi kuomba Rehema kwa Mungu, wakati huohuo unakisa naye.

*2. Sharti la Pili*

Baada ya kuungama pokea Ekaristi Takatifu, ili upate kuunganika na Kristo Mwana mpenzi wa Mungu.

Kutokupokea Ekaristi Takatifu ni kujitenga na Kristo; lakini Yesu mwenyewe alisema kuwa yeye ndiye njia kweli na uzima, mtu haji kwa Baba ila kwa njia yake.

Tunapokea Rehema kamili kwa njia ya Yesu Kristo peke yake.

Katika kuungama dhambi, liwe ni ungamo la kweli; katika ungamo la kweli mkristo aungamaye huwa hana kusudio la kutenda dhambi yoyote.

Inawezekana kabisa mtu akaja kutenda dhambi tena mara tu baada ya kuungama, lakini isiwe kwamba dhambi hiyo ilikuwa imekusudiwa kabla ya kuungama kwa mkristo huyo.

*3. Sharti la Tatu*

Chagua Sala au Tendo lolote utakalolifanya ili kujiletea Rehema Kamili.

*4. Sharti la Nne*

Usali sala ya Baba yetu mara moja, Salamu Maria mara moja, na Atukuzwe Baba mara moja kwa ajili ya nia za Baba mtakatifu.

*Aidha...*

Rehema Kamili hupatikana kupitia sala au Matendo yafuatayo .

1. Ibada ya Rozari Takatifu, walau moja.

Katika ibada hii hairuhusiwi kuikatisha kwa sababu yoyote ile.

Ikiwa mtu ataikatisha, basi atapaswa kuirudia upya.

2. Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ibada binafsi mbele ya Tabernakulo kwa muda
usiopungua nusu saa.

Katika ibada hiyo kinachotakiwa ni kutafakari zaidi, ambapo Mkristo aweza kuwa amesimama, au amepiga magoti, au ameketi mbele ya Tabernakulo.

3. Kusali njia ya Msalaba vituo vyote 14, au 15 pasipo kukatisha.

Baada ya ibada hiyo pia iunganishwe na Baba yetu moja, Salamu Maria mara moja, na Atukuzwe Baba mara moja, kwa ajili ya nia za Baba mtakatifu.

4. Fungua Biblia Takatifu kisha fungua mahali popote, chagua kifungu chohocte kisha kisome.

Hakikisha kuwa umekisoma na kukielewa kifungu hicho.

Usipokielewa kirudie tena na tena hadi ukielewe vema.

Baada ya hapo tafakari kwa nusu saa pasipo kuhamishahamisha mawazo.

Kisha hapo sali Baba yetu mara moja, Salamu Maria mara moja, na Atukuzwe Baba mara moja, kwa ajili ya nia za Baba mtakatifu.

5. Nenda hija ili kupata Rehema.

Hija si lazima kwenda nje ya nchi tu, bali ni mahali popote panapotambulika na Kanisa.

Makanisa yote ya Parokia ni moja ya vituo vya hija.

Aidha, rehema hii huwanufaisha watu wawili tu:

Yule aliyefanya ibada ya rehema hiyo,

Yule anayeombewa pia, hasa marehemu aliyeko toharani.

*REHEMA PUNGUFU*

Rehema pungufu hutoa msaada wa kupunguza baadhi ya malipizi kwa uule anayelengwa na ibada husika.

Inaitwa pungufu kwa sababu inalenga kumpunguzia adahabu, na hivyo kupunguza urefu wa muda wa kukaa toharani, iwapo kama yuko toharani.

Rehema pungufu inayo masharti yafuatayo:

1. Yule anaye Sali ili kuipokea asiwe na dhambi kubwa.

Dhambi kubwa kwa lugha nyingine ni dhambi ya mauti, ambayo mtu huipata kutokana na kuvunja kwa makusudi mojawapo ya amri yoyote ya Mungu, au ya Kanisa.

2. Anayesali ili kuipata anapaswa kuwa ametubu dhambi zake zote, na awe amejutia dhambi hizo, kiasi cha kumfanya asiwe na makusudio yoyote ya kuzirudia.

3. Sali au fanya ibada inayoleta Rehema pungufu.

Aidha, katika ibada za kuomba Rehema, tunaona sala kwa ajili ya kumuombea Baba mtakatifu zinapewa kiumbele kikubwa, je ni kwa nini?

Ni kwa sababu yeye ndiye anayeliongoza Kanisa la Mungu.

Kuomba Rehema pungufu kunatokana na kushindwa kutekeleza masharti ya kupata Rehema kamili, kwa sababu yoyote ile; ndiyo maana inaitwa Rehema pungufu.

*Kumbuka*

Katika kuhangaikia kutimiza masharti ya kupata Rehema kamili, lazima mwombaji
akutane na vikwazo mbalimbali.

Kikwazo chochote kinaweza kukuzuia kutimiza masharti ya kupata Rehema kamili.

Ni wajibu wa muimbaji wa Rehema kukishinda kikwazo hicho  kwani kushindwa huko kutamfanya mtu huyo kupata Rehema pungufu.

Mkristo daima anahimizwa kujijengea tabia ya kufanya mazoezi ya kiroho kama vile kujinyima ili kutoa sadaka, hasa kwa masikini na wahitaji mbalimbali.

Mkristo anatakiwa pia kujitahidi katika sala za mishale siku kwa siku.

Rehema kamili hupatikana mara moja tu kwa siku, isipokuwa kwa baadhi ya siku za pekee.

Siku zifuatazo zimewekwa na Kanisa kwa ajili ya Mkristo kujipatia Rehema.

1.Siku ambayo Mwanarozari  atajiunga rasmi na jumuiya ya Rozari Hai Ulimwenguni na saa ya kufa kwake.
2. Siku ya mwaka mpya, Kanisa limetoa Rehema kamili zaidi ya mara moja.

3. Katika siku za Ijumaa yoyote ya kwarezima Mkristo aweza kupata Rehema kamili zaidi ya mara moja.

4. Katika kipindi cha Wiki kuu na sherehe ya Pasaka pia kuna Rehema kamili zaidi ya mara moja kwa yeyote atakayetafuta.

5. Katika siku za sherehe ya Bwana yaani Utatu Mtakatifu, Ekaristi Takatifu, Moyo Mtakatifu wa Yesu, na Yesu Kristo Mfalme.

6.Katika Sikukuu ya Petro na Paulo Mitume.

7. Katika sikukuu ya somo wa Parokia.

8.Katika sikukuu ya Bikira Maria Malkia wa Ponsiunkula, Rehema kamili imetolewa kwa wale watakaosali katika Makanisa yote ya Parokia.

9. Siku za Mwezi wa kuombea marehemu wote, yaani kuanzia tarehe 1 hadi 8, za mwezi Novemba; atakayesali kuombea Marehemu atapata Rehema kamili.

Aidha  niwashauri Waamini wenzangu kujenga desturi ya kusali na kufanya mazoezi ya kiroho.