MAISHA YA WATAKATIFU
MT. YOHANE KRISOSTOMI,
ASKOFU NA MWALIMU WA KANISA
( 13 SEPTEMBA )
Yohane Krisostomi alizaliwa Antiokia (Uturuki) mwaka 349. 'Krisostomi' ni jina la kupanga, maana yake ni "Mwenye mdomo wa dhahabu", kutokana na mahubiri yake mengi yaliyoifafanua imani na kuhimiza maisha ya Kikristo. Baba yake alikuwa Mkuu wa Majeshi aliye shujaa; baba yake huyu alifariki dunia kabla Yohane hajapata kukua. Wakati huo, mama yake alikuwa na umri wa miaka ishirini tu. Ingawa alikuwa bado kijana, aliamua kukaa katika hali ya ujane kwa maisha yake yote na kumlea vizuri mwanae. Akafanya mpango ili apate kufundishwa na walimu mashuhuri.
Yohane alipanga urafiki na mmoja wa wanafunzi wenziwe, aliyekuwa akiita Basili. Kijana huyu alikuwa mwelekevu sana, kadhalika mwenye maadili mema, na alizidi kumvutia Yohane kwa mifano yake. Baada ya kufiwa na mama yake, Yohane alijitenga na watu, akakaa upweke pangoni, akiitunza roho yake kwa kusali na kufunga. Katika muda huo wote, alikuwa ameisoma sana Biblia kiasi cha kuisema yote kwa moyo, akafanya kozi ya Kichungaji kwa muda wa miaka kumi na miwili. Siku moja, aliteuliwa na watu wa Konstantinopoli (Uturuki) ili awe Askofu wao. Ijapokuwa Yohane hakukitaka cheo hicho, watu walimng'ang'ania tu, wakamchukua wakamweka garini na kumpeleka kwao.
Ingawa alikuwa mtu mwenye cheo, mazoezi yake yaliendelea kufuata mtindo ule ule wa zamani: alikula mara moja kwa siku, na kunywa maji tu; alilala kwa muda wa saa tatu au nne basi, na kusali kwa muda mrefu. Alikuwa na imani kubwa sana kwa Sakramenti ya Ekaristi. Alilichunga kundi lake kwa bidii: Wakristo waliokuwa wema waliimarishwa naye, na wale waliozipuuzia Amri za Mungu aliwakaripia kwa uzembe wao. Watu walimsikiliza kwa makini na furaha kwa vile alivyokuwa msemaji mashuhuri na mwenye moyo mwema. Lakini wale waliokuwa wamekewa naye kuhusu mwenendo wao mbaya, walimwonea na kumchongea kwa Kaisari. Hasa adui yake alikuwa Eudoksia, mkewe Kaisari, ambaye alikuwa mwanamke mwovu aliyeshirikiana na wafitini wa dini kuwanyang'anya mali zao na kuwadhulumu raia wenye kudai haki yao.
Mara ya kwanza, Askofu Yohane alipoondolewa na Kaisari kwenye madaraka ya Uaskofu na kuhamishwa kwa nguvu, Wakristo walilalamika sana kiasi cha kuwashurutisha wakuu wao wamruhusu Askofu wao arudi kwao. Alipokufukuzwa kwa mara ya pili, alikuwa ameukaribia uzee. Hata hivyo, askari waliamriwa kumpeleka mbali na kumsumbua njiani kadiri walivyoweza ili apate kufa upesi, kwa hiyo, askari hao walimlazimisha Askofu Yohane atembee kwa miguu, kila siku, mwendo mrefu, mchana kutwa akiwa juani, katika njia mbaya, na wakati walipoamua kupumzika, walifanya hivyo tu katika vijiji vile vidogo ambamo Askofu hangeweza kupewa huduma ya viburudisho. Hivyo, baada ya siku nyingi za mateso ya kila namna, ya njaa na kiu, Askofu Yohane akapata kufahamu ya kwamba nguvu zake zilikuwa zimemwishia. Alizimia njiani, akafa palepale, akisema: "Tumsifu Mungu siku zote". Huo ulikuwa mwaka 407. Umri wake ulikuwa miaka sitini.
MT. YOHANE KRISOSTOMI, UTUOMBEE
MASOMO YA MISA
I. 1Kor 12:12-14,27-31
Zab. 100
INJILI. Lk. 7:11-17